Serikali yasisitiza ubia kwenye sekta

Komentar · 128 Tampilan

Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kufikia dira 2050

*SERIKALI YASISITIZA UBIA KATI YA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI KUIFIKIA DIRA 2050.*

 

Serikali imesema itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ikiwemo miundombinu ya usafiri, kilimo, ufugaji, pamoja na sekta nyingine za maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali kwa wakati.

 

Hayo yalielezwa na Mchumi kutoka Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPU), Wizara ya Fedha, Bi. Josephine Melkiol, alipokuwa akieleza wananchi kuhusu majukumu ya kitengo cha PPP, waliotembelea katika Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane), yanayoendelea katika Uwanja wa Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.

 

Alisema Serikali imefanya maboresho ya Sera, Sheria na Kanuni za PPP ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo hadi Juni mwaka 2026, jumla ya mikataba tisa ya PPP imesainiwa kutoka sekta mbalimbali za maendeleo.

‘’Miradi iliyosainiwa ni Mabasi yaendayo kwa Haraka Dar Es Salaam (DART), awamu ya kwanza na ya pili yenye mikataba minne, ikiwemo Mradi wa Ukaguzi wa Lazima wa Vyombo vya Moto na Mradi wa Ujenzi na Uendeshaji wa Jengo la Biashara Kariakoo (DDC)’’, alisema Bi. Melkiol.

 

Alisema miradi mingine ni pamoja na Ukarabati na uendeshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), pamoja na Uboreshaji Bandari ya Dar Es Salaam kupitia kampuni za DP World na ADAN.

 

Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa njia ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), una tija kubwa ndio maana Serikali imeona umuhimu wa ushirikiano na sekta binafsi kama ilivyopewa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

 

‘’PPP ina faida nyingi sana ikiwemo kupata mtaji kutoka Sekta Binafsi na hivyo kupunguza utegemezi wa Bajeti ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo, kupata ujuzi, utaalamu na teknolojia kutoka Sekta Binafsi, kuwezesha upatikanaji wa ajira na mapato kwa Serikali, kuboresha upatikanaji wa huduma kwa ufanisi na kwa wakati pamoja na mgawanyo wa vihatarishi ambavyo kwa kiasi kikubwa vinabebwa na Sekta Binafsi’’ aliongeza Bi. Melkiol.

 

Maadhimisho ya Nane Nane 2026 yenye kaulimbiu ‘’ Tambua soko ongeza tija kuendeleza Dira 2050, ni Maadhimisho ya 33 ambayo yanalenga kukuza uchumi, kuongeza matumizi ya teknolojia bora na kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa ambayo yanaendelea katika Uwanja wa Nanenane jijini Dodoma.

Komentar